Tarehe 17 Januari 2025 Katibu Tawala Wilaya ya Nachingwea Ndg.Haji Balozi amefanya kikao na Maendeleo ya Jamii, viongozi wa chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Nachingwea.Lengo kuu la kikao kujadili mikakati ya kukuza sekta ya michezo na kuhamasisha fursa za kiuchumi kwa vijana.
Katika kikao hicho alieleza kuwa kwa muda sasa hakuna mpango wa kuboresha sekta ya michezo alikiri kuwa licha ya kuwa vijana wengi wanapenda michezo, hakuna sehemu maalum inayowaunganisha. Alisema, "Hakuna Ligi yoyote inayoendelea, na hili ni jambo la kuhuzunisha. Tunahitaji juhudi za pamoja ili kuimarisha michezo na kutoa fursa kwa vijana."
Ametoa maagizo kwa chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Nachingwea kuanzisha ligi na kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa ligi hiyo ili kuanza mara moja. Aidha, alisisitiza kuwa kila baada ya wiki mbili iwepo nafasi ya mabonanza ya michezo kwenye wilaya ili kuwahamasisha vijana na kuwaunganisha. "Tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja na viongozi wa timu zilizopo, ili kuhakikisha tunabuni njia bora ya kuinua michezo," alisema Katibu Tawala.
Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa Ofisi ya Maendeleo ya Jamii kuhamasisha vijana kuchukua mikopo ya 10% inayotolewa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, akiongeza kuwa hii ni fursa muhimu kwa vijana kuwekeza na kuboresha maisha yao.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.