Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Nachingwea imefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo, ikiwemo miradi ya afya, elimu na miundombinu ya barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 4.67.

Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nachingwea ndugu LONGINUS NAMBOLE, ambapo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

Mwenyekiti ameipongeza Wilaya na Halmashauri ya Nachingwea kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo, akieleza kuridhishwa na kasi pamoja na ubora wa ujenzi unaoendelea, hali inayoakisi matumizi sahihi ya fedha za umma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya wakandarasi, wataalamu na wananchi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni jengo la utawala ambalo limefikia asilimia 80 ya utekelezaji, barabara ya KKKT–Hospitali yenye urefu wa kilomita 0.5 iliyokamilika pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, kituo cha afya Chiola, kituo cha afya Nammanga pamoja na shule ya awali na msingi Stesheni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohammedi Hassan Moyo, amesema kuwa katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ataendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi thamani, ubora na ufanisi wa miradi yote ya maendeleo, ili fedha zilizotengwa ziwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.