Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango (FUM) ya Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Adinani Mpyagila, imefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 26 Januari, 2026, imehusisha miradi mitatu yenye thamani ya zaidi ya bil 1.2, Kamati imeeleza kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo, hususan katika ujenzi wa majengo yanayoendelea, na kuwasihi wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha wanatunza mazingira ya miradi hiyo.

Hata hivyo, kamati imebaini changamoto ya upatikanaji wa maji kujirudia katika miradi mingi, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa shughuli za ujenzi, Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri amewashauri madiwani kushirikiana na wananchi na viongozi wa maeneo husika ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unaimarishwa na kuepusha ucheleweshaji wa kukamilika kwa miradi.

Aidha, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Halmashauri, Rachel Lububu, akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri, amewataka watumishi wanaohusika na miradi hiyo kuhakikisha wanakuwepo mara kwa mara katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ili kusimamia shughuli zinazofanyika na kutatua changamoto za kiufundi zinazoweza kujitokeza kwa wakati.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.