Halmashauri ya Nachingwea imetenga kiasi cha shilingi 939,324,992.35 kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Fedha hizi zimetengwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, na vikundi vyenye sifa vinahimizwa kuwasilisha maombi yao kupitia ofisi za serikali za mitaa.
Vikundi vinavyotakiwa kuomba mikopo ni vile vilivyotambuliwa rasmi na halmashauri, vinavyojishughulisha na ujasiriamali mdogo au wa kati, au vinavyotarajia kuanzisha shughuli hizo. Vikundi vya wanawake na vijana vinapaswa kuwa na wanachama wasiopungua watano, wakati vikundi vya walemavu vinatakiwa kuwa na wanachama wasiopungua wawili.
Kwa kuongeza, vikundi vinavyohitaji mikopo vinatakiwa kuwa na akaunti ya benki kwa jina la kikundi kwa ajili ya matumizi ya shughuli za ujasiriamali. Wanakikundi wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wasio na ajira rasmi, wenye umri wa kuanzia miaka 18, huku wanachama wa vikundi vya vijana wakiwa na umri usiozidi miaka 45.
Maombi ya mkopo yanatakiwa kuwasilishwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa Halmashauri (mikopohalmashauri.tamisemi.go.tz), yakiambatanishwa na barua ya kikundi, muhtasari wa kikao cha kuomba mkopo, andiko la mradi, na taarifa ya akaunti ya benki ya kikundi.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.