Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Nachingwea Mhandisi Chionda M. Kawawa amefanya ziara ya kutembelea Mgodi wa Nditi na kukutana na kampuni ya Coast Nickel Industry Ltd inayofanya shughuli za uchimbaji katika Mgodi huo kwa sasa na itakayofanya uwekezaji Mkubwa Mgidini hapo kwa kushirikiana na Shirika la Umma linaloshughulika na uchimbaji, usimamizi, usindikaji na ukuzaji wa sekta ya madini nchini (STAMICO). Ziara hiyo imefanyika leo Novemba 18, 2025.

Katika ziara hiyo Mhandisi Kawawa ameitaka kampuni ya Coast Nickel Industry kufuata sheria za Nchi wakati wa utekelezaji wa kazi zao na pale watakapofanya uwekezaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jamii inanufaika na uwekezaji wao katika mgodi huo, utunzaji wa mazingira, kulipa kodi pia kuzingatia haki za binadamu kwani Wakazi wa Nditu na Nachingwea kwa ujumla wanategemea kuona wanapata maendeleo kupitia uwekezaji wao.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kawawa amewasihi wawekezaji hao kuhakikisha fidia za wakazi wa Nditi waliokua wanafanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo zinalipwa kwa wakati, kutengeneza mazingira ya ushirikiano kati yao na Halmashauri pamoja na Kata na kijiji pia ametoa agizo kwa Ofisi ya fedha ya Halmashauri ya Nachingwea kuhakikisha inawajengea uwezo Kata na Serikali ya Kijiji juu ya namna ya ukusanyaji wa mapato.

Aidha, Director wa Kampuni ya Coast Nickel Industry Ltd bwana Peter Ying na Share Holder wa STAMICO, amesema kama wawekezaji miongoni mwa malengo yao ni kuhakikisha uwekezaji Mkubwa unafanyika katika Mgodi huo ambao unatarajiwa kuazalisha zaidi ya tani 40,000 za Nickel kwa mwaka, pia watazingatia taratibj zote za uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi takribani 1,000 ambao wengi wao watakua ni wakazi wa Nachingwea, kulipa ushuru kwa Halmashauri, kuboresha miundombinu ya jamii na kuhakikisha utunzaji wa mazingira unafanyika.

Kwa upande wake mwakilishi wa STAMICO ndugu Ibrahim Dauda ambae ni Mining Manager wa shirika hilo, ameishauri Halmashauri kusimamia ukusanyaji wa Ushuru (Service Levy) kwa karibu na kwa kuzingatia leseni ya usafirishaji ya Mwekezaji ambayo ni ya tani 40,000.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.