Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo, Septemba 19, 2025 ameongoza uzinduzi wa kampeni kubwa ya chanjo ya mifugo wilayani humo, hatua inayolenga kupambana na magonjwa yanayoenezwa na mifugo kwenda kwa binadamu pamoja na kuwezesha utambuzi sahihi wa idadi ya mifugo.
Akizungumza katika viwanja vya Magereza, kijiji cha Chem Chem, Kata ya Stesheni, DC Moyo alisema kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha usalama wa afya za wananchi na ustawi wa mifugo, ambao ni tegemeo kubwa kwa maisha ya wakazi wa Nachingwea.
“Tunateka kuona mifugo yenye afya bora, bila magonjwa, na wafugaji wakiwa salama. Zoezi hili halitafanikiwa bila ushirikiano wenu. Hivyo nawahimiza mfanye kazi kwa karibu na maafisa mifugo katika kila kijiji,” alisema Moyo.
Kwa mujibu wa Afisa Mifugo wa Wilaya, Godfrey Mwina, kampeni hiyo inalenga kuchanja zaidi ya ng’ombe 5,000, mbuzi 24,000 na kuku 430,000. Hatua hiyo itasaidia kudhibiti magonjwa hatari yakiwemo ugonjwa wa mapafu kwa ng’ombe na kideli kwa kuku.
Wafugaji waliojitokeza katika zoezi hilo waliipongeza serikali kwa kuwajali na kuwatambua wafugaji wadogo, huku wakiomba maafisa mifugo kuendelea kufanya ziara za mara kwa mara vijijini ili kuwawezesha kupata msaada wa karibu.
Kampeni ya chanjo ya mifugo Nachingwea imeibua matumaini mapya kwa wafugaji, huku wengi wakiamini kuwa zoezi hilo litaboresha afya za mifugo yao na kuongeza tija kiuchumi kwa kaya zao.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.