Katika jitihada za kukuza kilimo nchini Tanzania, miche 5000 ya minazi na mbegu za ufuta, choroko na mbaazi imetolewa kwa wakulima katika vijiji 15 vya Wilaya ya Nachingwea. Zoezi hili limefanyika leo, likiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo, katika kijiji cha Mwenge, Kata ya Mitumbati.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo, amewashauri wakulima kuzingatia kilimo cha mazao ambayo yataweza kustahimili mabadiliko ya tabia nchi. Alisisitiza kuwa mbegu hizo zisifungiwe ndani bali zitumike ili kuleta tija kwa wakulima. Vilevile, amewaagiza maafisa ugani kuwatembelea wakulima na kuhakikisha hawakai ofisini.
Afisa Kilimo wa Wilaya ya Nachingwea, Raphael Ajetu, ametoa taarifa kuwa kuanzia mwaka 2025, zao la choroko litauzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, hatua ambayo itawawezesha wakulima kupata soko la uhakika.
Pia, kutokana na mabadiliko ya hali ya mvua, Afisa Kilimo Ajetu amesisitiza umuhimu wa wakulima kulima zao la mihogo kwa wingi katika mwaka 2025, kwani zao hili linastahimili ukame na lina umuhimu mkubwa katika kupunguza hatari ya njaa kwa wakulima wa Wilaya hiyo.
Wakazi wa kijiji cha Mitumbati, Yahaya Saidi na Salma Valence, wameishukuru Serikali kwa kuwajali katika utoaji wa miche hiyo na pia wameomba serikali kuendelea kuboresha sekta ya kilimo ili wanufaike zaidi. Wakulima ambao hawajapata miche hiyo wamehimiza juhudi za pamoja katika utunzaji wa miche ili kuhakikisha kila mmoja anafaidika. Kwa wale ambao hawajapata miche ya minazi, wanaweza kupokea mbegu za ufuta, choroko na mbaazi.
#Tupovizuri
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.