Katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea inakusudia kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi 40,595,578,276.00 kutoka vyanzo tofauti ndani ya Halmashauri hiyo na serikali kuu, bajeti imeongezeka kwa zaidi ya bilion 1 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/24 ambayo ilikua ni bilioni 38.8. Hayo yameelezwa kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya pili leo Januari 5, 2025.
Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo amesisitiza usimamizi wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya shule na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, pia, amewataka wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo kusimamia utolewaji wa stahiki za watumishi zipatikane kwa wakati ili waweze kusimamia na kutekeleza shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mheshimiwa Adinan Mpyagila ameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na amewaagiza waheshimiwa madiwani wote kusimamia wanafunzi wa kidato cha kwanza kwenda kuripoti kwa mwaka mpya wa masomo.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi ndugu Joshua Mnyanga'ali ameeleza kuwa kwa mwaka 2025 miradi yote ya maendeleo ikiwa ni pamoja na barabara, majengo ya zahanati ndani ya Wilaya ambayo ipo kwenye bajeti na ile ambayo bado haijatengewa bajeti inatarajiwa kukamilika ili kuendelea kukuza maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Mheshimiwa Amandus Chinguile pamoja na Katibu wa CCM Wilaya Mwanaisha Ame Mohamed wameipongeza Halmashauri kwa kutoa mikopo ya 10% ambayo inatokana na mapato ya ndani kwa wananchi na kutoa msisitizo katika ufuatiliaji wa marejesho ili kuwapa nafasi na wanufaika wengine waweze kupata mikopo hiyo kwa wakati.
Copyright ©2018 Nachingwea District Council. All rights reserved.